| Chapter 19 |
1 |
Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, "Haleluya! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu! --
|
2 |
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!" --
|
3 |
Wakasema, "Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!" --
|
4 |
Na wale wazee ishirini na wanne, na vile viumbe hai vinne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, "Amina! Asifiwe Mungu!" --
|
5 |
Kisha kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: "Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa." --
|
6 |
Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, "Haleluya! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Uwezo ni Mfalme! --
|
7 |
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa arusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari. --
|
8 |
Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung`aa!" (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watu wa Mungu.) --
|
9 |
Kisha malaika akaniambia, "Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!" Tena akaniambia, "Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu." --
|
10 |
Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunauzingatia ukweli ule alioufunua Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ukweli alioufunua Yesu ndio unaowaangazia manabii." --
|
11 |
Kisha nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpanda farasi wake aliitwa "Mwaminifu" na "Kweli". Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki. --
|
12 |
Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe. --
|
13 |
Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni "Neno la Mungu." --
|
14 |
Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na walikuwa wamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi. --
|
15 |
Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Uwezo. --
|
16 |
Juu ya vazi lake, na juu ya mguu wake, alikuwa ameandikwa jina: "Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana." --
|
17 |
Kisha nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, "Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu. --
|
18 |
Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapanda farasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa." --
|
19 |
Kisha nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi, pamoja na jeshi lake. --
|
20 |
Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka, pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake.) Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti. --
|
21 |
Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao. --
|