| Chapter 4 |
1 |
Mapigano na magombano yote kati yenu yanatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu. --
|
2 |
Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati, hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu. --
|
3 |
Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu. --
|
4 |
Ninyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu. --
|
5 |
Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: "Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa." --
|
6 |
Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: "Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu." --
|
7 |
Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni. --
|
8 |
Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki! --
|
9 |
Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa. --
|
10 |
Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni. --
|
11 |
Ndugu, msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali waihukumu. --
|
12 |
Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako? --
|
13 |
Basi, sasa sikilizeni ninyi mnaosema: "Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida." --
|
14 |
Ninyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Ninyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena. --
|
15 |
Mngalipaswa kusema: "Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile." --
|
16 |
Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya. --
|
17 |
Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi. --
|