| Chapter 10 |
1 |
Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. --
|
2 |
Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. --
|
3 |
Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. --
|
4 |
Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu. --
|
5 |
Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi." --
|
6 |
Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: `Nani atapanda mpaka mbinguni?` (yaani, kumleta Kristo chini); --
|
7 |
wala usiseme: `Nani atashuka mpaka Kuzimu` (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)." --
|
8 |
Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri. --
|
9 |
Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka. --
|
10 |
Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa. --
|
11 |
Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika." --
|
12 |
Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. --
|
13 |
Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa." --
|
14 |
Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? --
|
15 |
Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!" --
|
16 |
Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?" --
|
17 |
Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. --
|
18 |
Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu." --
|
19 |
Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu." --
|
20 |
Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu." --
|
21 |
Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii." --
|