| Chapter 4 |
1 |
Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. --
|
2 |
Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. --
|
3 |
Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate." --
|
4 |
Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Mtu haishi kwa mkate tu."` --
|
5 |
Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, --
|
6 |
"Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. --
|
7 |
Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu." --
|
8 |
Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."` --
|
9 |
Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, --
|
10 |
kwa maana imeandikwa: `Atawaamuru malaika wake wakulinde,` --
|
11 |
na tena, `Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."` --
|
12 |
Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Usimjaribu Bwana Mungu wako."` --
|
13 |
Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda. --
|
14 |
Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. --
|
15 |
Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote. --
|
16 |
Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. --
|
17 |
Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa: --
|
18 |
"Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, --
|
19 |
na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana." --
|
20 |
Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. --
|
21 |
Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo." --
|
22 |
Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?" --
|
23 |
Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: `Mganga jiponye mwenyewe`, na pia mtasema: `Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako."` --
|
24 |
Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake. --
|
25 |
Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote. --
|
26 |
Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni. --
|
27 |
Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria." --
|
28 |
Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana. --
|
29 |
Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini. --
|
30 |
Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake. --
|
31 |
Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato. --
|
32 |
Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha. --
|
33 |
Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio: --
|
34 |
"We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!" --
|
35 |
Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo. --
|
36 |
Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!" --
|
37 |
Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule. --
|
38 |
Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. --
|
39 |
Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia. --
|
40 |
Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. --
|
41 |
Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo. --
|
42 |
Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. --
|
43 |
Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo." --
|
44 |
Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea. --
|