| Chapter 4 |
1 |
Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. --
|
2 |
Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, --
|
3 |
"Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. --
|
4 |
Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. --
|
5 |
Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Mbegu hizo ziliota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. --
|
6 |
Jua lilipochomoza, zikachomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. --
|
7 |
Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. --
|
8 |
Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia." --
|
9 |
Kisha akawaambia, "Mwenye masikio na asikie!" --
|
10 |
Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. --
|
11 |
Naye akawaambia, "Ninyi mmejaliwa kujua siri ya Utawala wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, --
|
12 |
ili, `Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe."` --
|
13 |
Basi, Yesu akawauliza, "Je, ninyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? --
|
14 |
Mpanzi hupanda neno la Mungu. --
|
15 |
Watu wengine ni kama wale walio njiani ambapo mbegu zilianguka. Hawa hulisikia hilo neno lakini mara Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. --
|
16 |
Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu wanapolisikia hilo neno hulipokea kwa furaha. --
|
17 |
Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno mara wanakata tamaa. --
|
18 |
Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaolisikia hilo neno, --
|
19 |
lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. --
|
20 |
Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia moja." --
|
21 |
Yesu akaendelea kuwaambia, "Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa pishi au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. --
|
22 |
Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. --
|
23 |
Mwenye masikio na asikie!" --
|
24 |
Akawaambia pia, "Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. --
|
25 |
Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa." --
|
26 |
Yesu akaendelea kusema, "Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. --
|
27 |
Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. --
|
28 |
Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. --
|
29 |
Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika." --
|
30 |
Tena, Yesu akasema, "Tuufananishe Utawala wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? --
|
31 |
Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. --
|
32 |
Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake." --
|
33 |
Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. --
|
34 |
Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu. --
|
35 |
Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende ng`ambo." --
|
36 |
Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Palikuwapo pia mashua nyingine hapo. --
|
37 |
Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji. --
|
38 |
Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?" --
|
39 |
Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya! Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa. --
|
40 |
Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?" --
|
41 |
Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?" --
|