| Chapter 5 |
1 |
Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya. --
|
2 |
Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku. --
|
3 |
Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo. --
|
4 |
Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi. --
|
5 |
Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. --
|
6 |
Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. --
|
7 |
Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. --
|
8 |
Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma. --
|
9 |
Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, --
|
10 |
ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa. --
|
11 |
Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa. --
|
12 |
Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo. --
|
13 |
Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu. --
|
14 |
Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. --
|
15 |
Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. --
|
16 |
Furahini daima, --
|
17 |
salini kila wakati --
|
18 |
na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. --
|
19 |
Msimpinge Roho Mtakatifu; --
|
20 |
msidharau unabii. --
|
21 |
Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema, --
|
22 |
na epukeni kila aina ya uovu. --
|
23 |
Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. --
|
24 |
Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. --
|
25 |
Ndugu, tuombeeni na sisi pia. --
|
26 |
Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. --
|
27 |
Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. --
|
28 |
Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. --
|