| Chapter 4 |
1 |
Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo. --
|
2 |
Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu. --
|
3 |
Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea. --
|
4 |
Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu. --
|
5 |
Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. --
|
6 |
Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo. --
|
7 |
Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. --
|
8 |
Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; --
|
9 |
twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa. --
|
10 |
Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu. --
|
11 |
Naam, katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa. --
|
12 |
Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi. --
|
13 |
Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena. --
|
14 |
Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. --
|
15 |
Yote haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu. --
|
16 |
Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. --
|
17 |
Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. --
|
18 |
Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele. --
|